WE ARE UNDER CONSTRUCTION........COMING BACK SOON
Most Popular

Jumanne, 14 Juni 2016

Upelelezi wa Kesi ya Rushwa Inayowakabii Wabunge wa CCM Wakamilika

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa (Takukuru), imekamilisha upelelezi wa kesi ya rushwa inayowakabili wabunge watatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wabunge hao wa CCM ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ni Ahmed Saddiq (Mvomero), Kangi Lugola (Mwibara) na Victor Mwambalaswa (Lupa).

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Godliver Kiriani aliiambia mahakama ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na aliomba ipangwe tarehe kwa ajili ya kuanza kuwasomea washtakiwa maelezo ya kesi inayowakabili.

Hakimu Simba alipanga kesi hiyo ianze kusikilizwa Julai 4 baada ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washtakiwa hao ambao hadi jana hawakuwa na mawakili, wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza sharti la kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya Sh5 milioni.

Wabunge hao walipandishwa kizimbani na Takukuru kwa mara ya kwanza Machi 31, 2016 na kusomewa mashtaka na wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo.

Washtakiwa hao wanadaiwa kwa nafasi zao za ujumbe wa LAAC, waliomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Mbwana Magote ili waweze kutoa mapendekezo mazuri ya Taarifa ya Hesabu za halmashauri hiyo za mwaka 2015/2016.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Machi 15, 2016, kinyume cha kifungu cha 15 (2) cha Sheria ya Takukuru, wakiwa katika Hotel ya Golden Tulip, iliyoko eneo la Masaki, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam