Prof. Ibrahim Lipumba, aliye jihudhuru uwenyekti wa Chama cha Wananchi (CUF) ametangaza nia yake ya kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti-taifa wa chama hicho.
Amesema, anarejea kwenye nafasi hiyo baada ya muda wa kutosha alioutumia kutafakari siasa za nchini na namna demokrasia inavyokiukwa na watawala wa nchi hii.
“Nimemwandikia Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) kutengua barua yangu niliyoandika 5 Agosti mwaka jana,” amesema Prof. Lipumba.
Prof. Lipumba alijiuzulu nafasi yake mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumridhia Edward Lowassa kupeperusha bendera ya umoja huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kupitia Chadema.
Hata hivyo amesema, analazimika kurejea kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa kutokana na kuguswa na matatizo ya demokrasia nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam amesema kuwa, amemuandikia barua Maalim Seif ili atengue uamuzi wake wa awali wa kuachia nafasi hiyo.
Katiba ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inaeleza kwamba, barua ya kujiuzulu inapaswa kujadiliwa na Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika.
Prof. Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999. Ibara hiyo inaipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake na kwamba, kauli yake ya leo kuwa Maalim Seif atengue barua yake inatokana na kutokwenda kwenye ngazi hiyo (Mkutano Mkuu) nyingine ya uamuzi.