Watu watatu wamepigwa risasi na kufa leo mjini Nairobi, polisi walipokuwa wanawatawanya maelfu ya wafuasi wa upinzani waliokuja kummpokea kiongozi wao Raila Odinga aliyerejea nyumbani kutoka ughaibuni. Watu hao watatu, ambao ni wanaume, miili yao imeonekana barabarani huko Muthurwa, kitongoji kilichoko kwenye mji mkuu ambako polisi waliokuwa na hewa za kutoa machozi na mabomba ya maji na bunduki za rashasha walikabliana na waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe. Raila odinga amerejea nyumbani leo baada ya ziara ya siku kumi nchini Marekani na Uingereza ambako alikwenda kutafuta uungaji mkono wa madai yake kutaka uchaguzi wa rais urudiwe upya nchini Kenya.