Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange amewataka wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi za kusini mwa Afrika (SADC), kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kwenye Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC) kuboresha majeshi yao.Alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki alipokuwa akitoa vyeti kwa maofisa wa jeshi 37 waliohitimu kozi maalumu ya ukamanda na unadhimu.
Alisema wanajeshi wa EAC na SADC wanapaswa kuhakikisha wanatumia weledi pamoja na mbinu mbalimbali walizozipata kwa ajili ya kuleta ufanisi jeshini pamoja na kuhakikisha wanawezesha jeshi kuwa na maendeleo.Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC), Brigedia Jenerali Sylvester Minja alisema wanajeshi hao wamehitimu kozi maalumu ya ukamanda na unadhimu.Alisema wahitimu 25 wametoka hapa nchini.
Nchi nyingine ambazo zilikuwa na askari wawili kila moja ambayo askari wake walihudhuria mafunzo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Zimbabwe na Zambia. Kwa upande Burundi na Namibia, zilikuwa na askari mmoja kila moja. Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Wilson Nkambaku.Chuo hicho kilianza kutoa mafunzo yake Julai mosi mwaka jana mara baada ya kuhamia kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Tanzania (TMA) kilichopo wilayani Monduli mkoani Arusha.
Chuo hicho kimetajwa kuwa na mafanikio kwa kusimamia na kuendesha mafunzo yake kwa kutumia maofisa watanzania.
Kimeanzisha stashahada na astashahada katika elimu ya statejia iliyoanza rasmi mwaka 2013 kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Njiro.