Australia imetangaza kuanza uchunguzi wa mabaki ya ndege yaliyogunduliwa kwenye kisiwa kidogo cha Kojani, visiwani Zanzibar, kutambuwa endapo ni ya ndege ya Malaysia, nambari MH370, ambayo ilipotea Machi mwaka 2014, ikiwa na watu 239.
Waziri wa Usafirishaji wa Australia, Darren Chester, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mabaki hayo, lakini mwanzoni mwa mwezi huu, wavuvi kwenye kisiwa cha Kojani waligundua kile wanachoeleza kuwa ni bawa la ndege, ambalo bado linaendelea kushikiliwa huko.
Waziri Chester amesema tayari mamlaka nchini Malaysia zimefanya mawasiliano na wenzao wa Tanzania kupanga namna ya kuyachunguza mabaki hayo. Mwezi Mei, vipande vyengine vinavyokisiwa kuwa mabaki ya ndege hiyo, viliokotwa kwenye visiwa vya Reuniun na Mauritius. Australia inaendesha operesheni kubwa kuisaka ndege hiyo kwenye eneo la kusini mwa Bahari ya Hindi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 105,000.