Uhakiki mpya wa watumishi wa umma uliofanywa mkoani Mwanza umebaini watumishi hewa 1,057 na kuiingizia Serikali harasa ya Sh2.1 bilioni.
Miongoni mwa watumishi hao wamo watoro, wastaafu, waliofukuzwa, waliofariki, wasiojulikana kwa mwajiri na walioacha kazi na kujiingiza kwenye siasa lakini wanaendelea kulipwa mishahara.
Idadi hiyo ya watumishi hewa imebainika katika uhakiki uliofanyika kati ya Aprili 18 hadi Juni 3, baada ya ule wa awali kuwanasa 334.
Akitoa taarifa ya uchunguzi ulioshirikisha vyombo vya dola na mamlaka nyingine za Serikali, Mkuu Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema: “Niliagiza uhakiki ufanyike upya na watumishi wote waliokuwa masomoni, likizo au safari kurejea kwenye vituo vyao vya kazi kuhakikiwa kwa picha na nakala za miezi mitatu iliyopita ya malipo ya mishahara.”
Mongella alisema watumishi 214 wamebainika ni watoro lakini Serikali imewalipa zaidi ya Sh1.5 bilioni huku wastaafu 10 wakiendelea kulipwa zaidi ya Sh54.3 milioni kutokana na majina yao kuwapo kwenye orodha ya malipo.