Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limewasimamisha wabunge wa wawili Mh Suzani Lyimo na Anatropia Theonest wote wakiwakilisha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)kushiriki katika vikao nane vya bunge baada ya kubainika kuwa walisema uwongo bungeni.
Maamuzi hayo yalifikiwa baada ya kamati haki,maadili na madaraka ya bunge kufanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa wabunge hao walitoa taarifa za uwongo bungeni dhidi ya waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi,Mh Wiliam Lukuvi na Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh Hamad Masauni ambapo Mh Lyimo kafungiwa kushiriki vikao vitano na Mh Anatropia vikao vitatu.
Hatua hiyo inapingwa vikali na Mh James Mbatia Mbunge wa Vunjo ambaye anasema japo bunge linaongozwa kwa sheria na kanuni Naibu spika Dk Tulia Ackson hakupaswa kubariki jambo hilo kwani ni kuongeza mpasuko baina ya wapinzani na kiti.
Wakati wapinzani wakisema hivyo wabunge wa Chama Tawala CCM wamesema ni lazima wabunge wa upinzani wajue zipo sheria zinazoliongoza bunge hilo na jambo la msingi ni wao kuzifuata la sivyo watajikuta wanapewa adhabu kila siku.
Bunge limehitimisha sehemu yake ya kwanza ya mjadala wa bajeti ambapo Mh Atupele Mwakibete Mbunge wa Busekelo amesema ni matumaini ya wabunge kuwa wakati atakapokuja kujibu hoja zao atafanya marekebisho mengi kama wabunge walivyoshauri.