Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imemkabidhi Rais John Magufuli hundi ya Shilingi Bilioni 12 zilizobaki kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuokoa fedha hizo na kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine na ametaka taasisi nyingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi ya taifa.
Pamoja na kukabidhi hundi ya baki ya shilingi Bilioni 12, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amemuomba Rais Magufuli aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi , kwa kuwa hivi sasa tume inatumia majengo ya kupanga ambayo yanaigharimu tume hiyo takribani shilingi Bilioni 1 na Milioni 400 kila mwaka ,kwa kulipia kodi ya pango, usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.
Rais Magufuli pia amelikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa kwa mfuko wa tume ya uchaguzi ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata, badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za kugharamia uchaguzi huo.