Sakata la mkopo wa Serikali wa dola milioni 600 za Kimarekani uliohusisha benki za Stanbic Tanzania na Standard Bank PLC ya Uingereza limetinga bungeni baada ya upinzani kuhoji sababu za baadhi ya watuhumiwa kutofikishwa mahakamani.
Sakata hilo, ambalo hivi sasa liko mahakamani linahusisha watuhumiwa watatu, ambao ni mkurugenzi wa kampuni ya Egma, Harry Kitillya na maofisa wawili wa zamani wa Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.
Msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde aliibua sakata hilo katika maoni ya bajeti yake alipohoji Standard Bank kuhusishwa kutokana na ukweli kwamba aina ya mkopo ambao Serikali ilikuwa inautaka hauwezi kutolewa na Stanbic Tanzania kwa kuwa haina huduma hiyo.