Rais wa Marekani, Barack Obama, ameshtumu vikali matamshi ya mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, kwamba waislamu wasiruhusiwe kuingia Marekani. Obama amesema hiyo 'si marekani wanayohitaji.'
''Kuwabagua Waislamu wa Marekani kutasababisha nchi hiyo kukosa usalama,na kuongeza tofauti iliopo kati ya nchi za magharibi na zile za kislamu'', Obama alisema
Siku ya Jumatatu bwana Trump, aliongezea kuhusu mpango wa kupiga marufuku nchi zote ambazo zina historia ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya Marekani.
Alisema shambulio la ufyatuliaji risasi la Orlando linathibitisha yote.
Watu 49 waliuawa, baada ya Omar Mateen raia wa Marekani ambaye wazazi wake ni raia wa Afghan kufyatua risasi katika kilabu ya wapenzi wa jinsia moja huko Orlando.
Bwana Trump amesema pendekezo lake litatekelezwa kupitia (uamuzi wa pamoja ) iwapo rais atapewa mamlaka ya kupiga marufuku uingizaji wa watu wenye daraja lolote katika nchi hiyo jambo ambalo rais ataliona kuleta madhara ya kiusalama kwa Marekani.
Lakini siku ya Jumanne katika wizara ya fedha mjini Washington,Obama aliyekuwa amekasirishwa na matamshi hayo ya Trump alimshambulia mgombea huyo anayetarajiwa kuthibitishwa kuwa mteuzi wa urais wa chama cha Republican mwezi ujao.