Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya yameshutumu maafisa wa polisi wakisema walitumia nguvu kupita kiasi kukabili waandamanaji jijini Nairobi Jumatatu.
Tume ya Taifa ya Haki za Kibinadamu (KNHRC) imesema imeshangaza sana na video na picha ambazo zinaenea kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri wakati wa maandamano hayo.
Picha hizo zinawaonesha polisi wakiwakabili waandamanaji kwa marungu. Baadhi ya wakenya mtandaoni pia wamekuwa wakiwashutumu maafisa wa polisi na kitambulisha mada #StopPoliceBrutality (Komesha Ukatili wa Polisi) kinavuma Kenya.
Kwa Picha: Maandamano ya upinzani Nairobi
Kwa mujibu wa kituo cha redio cha Capital FM jijini Nairobi, mmoja wa waliokabiliwa na polisi alifariki baadaye akipokea matibabu.
"Kikosi cha Polisi ni kikosi cha nidhamu na si kikosi cha kutumia nguvu. Kanuni ziko wazi kuhusu jinsi ya kuwashughulikia raia wakati wa maandamanaji,” tume hiyo imesema kupitia Twitter.
Mamlaka huru ya kiraia inayofuatilia shughuli za polisi (IPOA) pia imeshutumu vitendo vya maafisa wa polisi na kusema walivuka mipaka.
Mwenyekiti wa mamlaka hiyo Bw Macharia Njeru amewaambia wanahabari kwamba polisi walitumia nguvu kupita kiasi.
Amesema maafisa wa mamlaka hiyo wanakamilisha uchunguzi na watawasilisha ripoti kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili hatua zichukuliwe dhidi ya maafisa husika.
Muungano wa upinzani CORD umekuwa ukifanya maandamano Jumatatu kila wiki kuwashinikiza maafisa wakuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) wajiuzulu.
Viongozi wa CORD wamesema maafisa hao hawawezi kusimamia uchaguzi huru na wa haki wakati wa uchaguzi mkuu ujao 2017.
Wameahidi kuendelea na maandamano hayo hadi maafisa hao watakapong’atuka