WE ARE UNDER CONSTRUCTION........COMING BACK SOON
Most Popular

Ijumaa, 18 Machi 2016

Mkurugenzi Rubada kizimbani kwa wizi

KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo
ya Bonde la Rufiji (Rubada), Aloyce Masanja,
amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi
na utakatishaji wa Sh milioni 86.
Mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Mshtakiwa Masanja alisomewa mashtaka manne
yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu, Waliyarwande Lema.
Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Joseph
Kiula akisaidiana na Denis Lekayo, walidai
mahakamani kwamba kati ya Agosti mosi hadi
10, 2010 katika Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa
huyo akiwa mtumishi wa Serikali na wadhifa
alionao aliiba Sh milioni 50 zilizofika kwake
kulingana na nafasi yake ya ajira.

Katika shtaka la pili inadaiwa Masanja kati ya
Novemba 10 hadi 30, 2010 aliiba Sh milioni 36
zilizofika kwake kulingana na nafasi yake ya
ajira.
Kiula alidai katika shtaka la tatu na la nne,
mshtakiwa anatuhumiwa utakatishaji wa fedha
jumla ya Sh milioni 86 baada ya kujiingiza
katika uhamishaji wa fedha hizo huku
akifahamu kwamba fedha hizo ni zao la kosa la
wizi.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo huku
upande wa mashtaka ukidai upelelezi wa kesi
hiyo umeshakamilika.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 24 mwaka huu
mshitakiwa huyo atakaposomewa maelezo ya
awali pamoja na kuangalia kama anaweza
kupata dhamana ama la.