WE ARE UNDER CONSTRUCTION........COMING BACK SOON
Most Popular

Jumatano, 29 Juni 2016

Watu 5 wamefariki dunia na 13 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Super Sami mkoani Mwanza.


Abiria watano waliokuwa wakisafiri kwa basi la Super Sami kutoka jijini Dar es Salaam kwenda jijini Mwanza wamefariki dunia papo hapo na wengine kumi na tatu kujeruhiwa vibaya baada ya basi hilo kugonga jiwe na kupinduka katika eneo la Bushini kata ya Mabuki wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Juni 28 majira ya saa saba usiku ambapo dereva wa basi hilo William Elias na msaidizi wake ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha.

Amesema basi hilo lenye namba za usajili T.449 BCB aina ya Zhongtong liligonga jiwe lililokuwa barabarani, hali iliyopelekea dereva kushindwa kulimudu na kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi 13 ambao wamekimbizwa katika hospitali ya rufaa Bugando na hospitali ya wilaya ya Misungwi kwa ajili ya matibabu.

Kamanda Msangi amewataja waliofariki dunia kuwa ni Vaileth Odede mkazi wa Mwanza, mwanaume mmoja na wanawake wawili ambao majina yao hayajatambuliwa hadi sasa wanaokadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30.

Kwa upande wa majeruhi, kamanda huyo wa polisi mkoani Mwanza kamishna msaidizi mwandamizi Ahmed Msangi amewataja kuwa ni Sophia Miraji, Kibilo Mwacha, Boniphace Charles, Frank Munyumi, Stanley Zacharia, Sia Dauson, Hellen Leheke, Michael Leonard, Zamda Issa, Marietha Chrisper, Elizabeth Simon, Dickson Msamba na Kudra Ibrahim ambaye ni mtoto mwenye umri wa miaka miwili na miezi sita.