WE ARE UNDER CONSTRUCTION........COMING BACK SOON
Most Popular

Jumanne, 12 Aprili 2016

Moto wateketeza maduka 150 mkoa wa Kagera

Moto mkubwa umezuka na kuteketeza vibanda vya maduka
zaidi ya 150 katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoa
wa Kagera magharibi mwa Tanzania.

Moto huo ambao
ulianza Jumatatu majira ya sa 2:00 usiku umeteketeza mali
na bidhaa za aina mbalimbali kama mchele, sukari, nguo,
simu, pamoja na bidhaa zingine.

Wananchi wa Karagwe imewapasa
kusubiri gari la Zimamoto kutoka Bukoba Mjini (magari ya
uwanja wa ndege) ambako ni kilomita 120 kufika karagwe
mjini. Hata hivyo magari hayo yalikuta maduka mengi
yamekwishateketea.

Diwani wa kata ya Kanoni wilaya karagwe Sabi Rwazo
amesema tukio hilo limewastua na ni tukio la kwanza la
moto kuunguza soko wilayani humo. Anasema tatizo la
ukosefu wa gari la zima moto linachangiwa na uhaba wa
fedha. “Mara nyingi katika bajeti yetu imekuwa ikishindwa
kununua gari.” Amesema Rwazo na kusema maombi yao
yako serikali kuu.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Deodatus Kinwiro amesema
kuwa Serikali ya wilaya yake itapata gari la zima moto hivi
karibuni, “Bahati nzuri nilikuwa Dar es Salaam, nimekutana
na kamishna mkuu wa zima moto ameniahidi kunipatia gari
jipya,” amesema Kinwiro na kuongeza kuwa, “wakati wowote
gari hilo litafika wilayani Karagwe.”

Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema hawakubaliani na
kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kwa sababu wamekuwa
wakitozwa kiasi cha TZS 30,000 kwa mwezi ili kuchangia
huduma za zimamoto wilayani hapo lakini wanashangaa kwa
nini hawapati elimu ya kujikinga na majanga, na hakuna hata
gari la dharura.

Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana lakini taarifa
za awali zimeonesha kuwa kuna Mamalishe mwenye kibanda
sokoni hapo aliacha jiko lake bila kuzima hivyo likashika nguo
zilizokuwa katika kibanda hicho na kusababisha moto
kusambaa ghafla.