Serikali imerasimisha jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa ni siku ya usafi kitaifa kupitia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kifungu 191 ambapo mtu yeyote atakayekaidi kufanya usafi siku hiyo atatozwa faini isiyopungua shilingi elfu hamsini au kifungo cha kuanzia miezi mitatu mpaka miaka saba na atakayebainika kutupa taka hovyo atatozwa shilingi laki mbili papo hapo na kwa kampuni au taasisi italipa milioni tano na kuendelea.
Akitangaza kurasimishwa kwa siku hiyo katika zoezi la usafi wa lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Naibu waziri ofisi Makamu wa Rais Muungano na mazingira Mhe Luhaga Mpina amesema serikali imeridhia iwe maalum kwa ajili ya usafi ambapo utekelezaji wake utasimamiwa na viongozi kuanzia ngazi za chini kupitia muongozo wa tangazo la serikali kupitia gazeti lake namba 139/2016 la tarehe 23 aprili mwaka huu.
Awali zoezi hilo almanusura liingie dosari ambapo wanafunzi wanaosomea astashahada ya ualimu kumvamia waziri Mpina wakidai hawajafundishwa kwa muda wa mwezi mmoja kufuatia mgomo wa walimu na kumzuia waziri huyo kufanya kilichompeleka wakidai mpaka afike waziri wa elimu sayansi na teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kusikiliza madai yao.
Kufuatia hali hiyo hali ikamlazimu waziri Mpina na baadhi ya wabunge alioambatana nao akiwemo mwenyekiti wa kamati ya bunge ya viwanda biashara na mazingira ambaye pia ni Mwalimu wa nje wa chuo hicho Mhe Dalali Kafumu kutuliza hali ya hewa kwa kuwaahidi wanafunzi hao kulifikisha suala hilo pahala husika.