WE ARE UNDER CONSTRUCTION........COMING BACK SOON
Most Popular

Jumanne, 26 Aprili 2016

Rais John Pombe Magufuli avunja bodi ya mamlaka ya mawasiliano Tanzania (T.C.R.A)

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli ameivunja Bodi ya
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na
kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Ally Yahaya Simba.

Taarifa kutoka Ikulu imesema Bw Simba amesimamishwa
kazi kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa
utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS).

Bodi ya TCRA imekuwa ikiongozwa na Prof Haji Semboja. Taarifa hiyo inasema hatua hiyo ilisababisha Tanzania
kupoteza mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu tarehe 22 Machi, 2013.

Kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), kwa mujibu wa serikali.

Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.

Aidha, amewataka Waziri Prof Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za
ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.

“Nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na
sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote atakayekwamisha
jambo hili,” amesema Rais Magufuli.